1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baa la njaa kuathiri Sudan Kusini

15 Agosti 2014

Ni wazi kuwa muda mwingine wa mwisho uliowekwa kufikia makubaliano ya amani umepita, na badala ya kuleta amani, viongozi wa pande mbili nchini humo wanaendelea kuitumbukiza nchi hiyo katika baa la njaa.

https://p.dw.com/p/1CvXx
Flüchtlingslager im Südsudan 01.08.2014
Wakimbizi wa Sudan KusiniPicha: Charles Lomodong/AFP/Getty Images

Jumapili iliyopita ndio ulikuwa mwisho kwa wawakilishi wa Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamo wake Riek Machar kuwasilisha pendekezo la mwisho la kuunda serikali ya mpito ambayo inazijumuisha pande zote zenye lengo la kumaliza machafuko yaliyodumu miezi minane. Hata hivyo jambo hilo halikuwa na msaada wowote wenye kuleta mabadiliko, na badala yake, kilichofuatia ni mapigano zaidi nchini humo.

Kila pambano jipya ambalo limekuwa likitokea nchini humo, huchochea hali ya usalama wa chakula, ambapo Jumuiya ya kimataifa ilionya kuwa, tatizo la baa la njaa huenda likadumu hadi Desemba.

Zaidi wa watu milioni moja wanakabiliwa na baa la njaa

Flüchtlingslager im Südsudan 01.08.2014
Mtoto wa Sudan KusiniPicha: Charles Lomodong/AFP/Getty Images

Jumuiya hiyo imeeleza kuwapo watu milioni 1.1wanaokabiliwa na tatizo la njaa, huku ikiripotiwa kuwa, mpaka mapigano hayo yatakapoisha, mawakala wa misaada hawataweza kuwafikia maelfu ya watu, ambao wangehitaji kupatiwa msaada.

Mpaka sasa hakuna dalili yeyote ya kusitishwa mapigano hayo. Mapema wiki hii, wakati wa ziara ya ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, Balozi wa Marekani Samantha Power aliielezea ripoti waliyoipokea, kwamba askari wengi zaidi wamepelekwa nchini Sudan Kusini ili kutengeneza mazingira kwa vita vingine.

Wakati huo huo, mapema Agosti, wanamgambo wa kundi la kijeshi, kundi ambalo linafanya kazi zake nje ya amri ya jeshi la Serikali ama kwa waasi, liliwauwa wafanyakazi sita wa mashirika ya misaada katika maeneo ya Upper Nile, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Sudan. Waliamua malengo yao kulingana na uhusiano wa kikabila, kuendeleza mgawanyiko wa kikabila ambao ndiyo chanzo hasa cha mgogoro huu.

Kiini cha machafuko

Mgogoro huo wa miezi minane ulianza kama mgogoro wa kisiasa kati ya Kiir na Machar juu ya nani atakayekiongoza chama cha Sudan People´s Liberation Movement. Hali hiyo iliongeza mvutano wa kikabila baada ya mgogoro huo kusambaa zaidi hadi kufikiaa nusu ya mashariki ya nchi hiyo, ambapo ukiukwaji wa haki za binadamu ukawa moja ya chanzo cha mgogoro mkubwa.

Vurugu hizo ambazo zimekuwa ni suala la kawaida katika maeneo makubwa nchini humo, ambayo mauwaji yake yamewalenga zaidi wafanyakazi wa mashirika ya misaada na watu wa kabila la Nuer wanaoishi Upper Nile katika kaunti ya Maban, huenda zikawa chanzo kikubwa cha kuongeza ukali wa migogoro inayoendelea.

Maban ni sehemu ambayo inahifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka nchini Sudan, imekuwa ni sehemu ambayo haijakumbwa kwa kiasi kikubwa na mapigano hayo. Lakini, hawakuacha kutumia kikundi cha ndani cha wanamgambo wao, ambao wenyewe wamekuwa wakijiita kikundi cha kijeshi cha Maban ambacho kinajitegemea pasipo kuegamia upande wowote.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini umeonya katika vyombo vya habari na kueleza kuwa, mji wa Maban ulikuwa hatarini kutumbukia katika ukosefu wa utawala wa sheria ambao bila makubaliano halali ya amani unaweza kusaambaa katika maeneo mengine ya nchi wakati ambapo jamii zitakapoamua kuanza kutekeleza haki kwa njia zao wenyewe.

Mwandishi: Happiness Matanji
Mhariri: Saumu Yusuf