1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yaidhinisha kikosi dhidi ya Boko Haram

30 Januari 2015

Umoja wa Afrika - AU umeidhinisha mpango wa kuweka kikosi cha kikanda chenye wanajeshi 7,500 kwa ajili ya kupambana na kundi lenye itikadi kali ya kiislamu la Boko Haram la nchini Nigeria.

https://p.dw.com/p/1ETHt
Chumba cha mkutano cha Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa
Chumba cha mkutano cha Umoja wa Afrika mjini Addis AbabaPicha: AFP/Getty Images

Kuidhinishwa kwa mpango wa kuundwa kwa kikosi hicho kumetangazwa na kamishna wa baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika, Smail Chergui, akizungumza na waandishi wa habari pembeni mwa mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi wanachama wa umoja huo mjini Addis Ababa.

Akizungumza awali katika kikao cha baraza hilo, mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma alisema ukatili unaofanywa na kundi la Boko Haram, ambao haujali hata kidogo maisha ya binadamu na mali zao, unazusha wasiwasi mkubwa. Bi Zuma alisema ghasia zinazoendeshwa na kundi hilo kaskazini mashariki mwa Nigeria na katika eneo zima la ziwa Chad, ni kitisho kinachoweza kueneza machafuko katika kanda nzima.

Wanajeshi 7,500 kutoka nchi tano

Nchi za ukanda unaokabiliwa na kitisho cha Boko Haram zilikuwa zimetoa ahadi ya kila moja kuchagia kombania kwenye kikosi cha pamoja, ambao jumla yao ingekuwa takribani wanajeshi 3000, lakini mkuu wa Halmashauri ya Afrika alipendekeza idadi hiyo iongezwe hadi angalau askari 7,500.

Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Afrika, Nkosazana Dlamini Zuma
Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Afrika, Nkosazana Dlamini ZumaPicha: picture-alliance/dpa/ Y.Valat

Kikosi kilichoidhinishwa kitapewa muda wa awali wa mwaka mmoja kuendesha operesheni zake, na inaaminika kuwa kitapata uungwaji mkono wa kimataifa. Nchi zilizokubali kuchangia wanajeshi katika kikosi hicho ni Nigeria, Cameroon, Chad, Niger na Benin. Maafisa wakuu wa AU wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wanajeshi wa kila nchi watabaki nchini mwao, na kwamba operesheni zao zitakuwa zikiratibiwa kwa pamoja kutoka mji mkuu wa Chad, N'Djamena.

Kanda ikitaka msaada, AU itaridhia

Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma amesema ikiwa nchi hizo zitahitaji msaada zaidi, Umoja wa Afrika utatafakari cha kufanya.

''Nchi za kanda zimechukua uamuzi juu ya namna ya kuipiga vita Boko Haram. Sisi tutaunga mkono uamuzi wao, lakini ikiwa watahitaji msaada zaidi kutoka nje ya kanda yao, sina shaka lolote Umoja wa Afrika utatafakari hatua muafaka za kuchukuliwa''. Amesema Bi Zuma.

Ingawa Kitisho cha Boko Haram ndicho agenda kuu ya mkutano huu wa wakuu wa mataifa wanachama wa AU, yapa masuala mengine ambayo yatapewa kipaumbele. Uchaguzi wenye amani ni mojawapo ya masuala hayo, ikizingatiwa kuwa nchi zaidi ya kumi wanachama wa umoja huo zitafanya uchaguzi mkuu mwaka huu.

Hali kadhalika mogogoro ya vita inayoendelea nchini Sudan Kusini na katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambazo zote zinatarajiwa kufanya uchaguzi mwaka huu, ni suala jingine ambalo mkutano huo wa Addis Ababa hauwezi kulifumbia macho. Mzozo mwingine unaotokota ambao bila shaka utakuwa katika agenda ya mazungumzo ni ule wa Libya.

Viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika vile vile wanatarajiwa kujadili uchumi wa nchi zilizoathiriwa vibaya na maradhi ya Ebola, na kuunda fuko la mshikamano na kupendekeza kuwepo kwa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti Magonjwa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri:Josephat Charo