1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

11 Julai 2014

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yamezungumzia juu ya wahamiaji haramu wa Kiafrika na changamoto wanazotoa kwa Italia, miaka mitatu ya uhuru wa Sudan Kusini na matumaini ya amani Jamhuri ya Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/1CbFP
Symbolbild Flüchtlinge Sizilien Bootsflüchtlinge
Picha: picture-alliance/AP Photo

Kwenda mbinguni kupitia jahannam
Watu zaidi na zaidi wanakimbia Afrika kuelekea barani Ulaya kupitia bahari ya Mediterrani. Wiki iliyopita pekee, vikosi vya usalama vya Italia viliwaoko wahamiaji haramu 2600 wa Kiafrika. Watu hao waliokuwa katika mashua saba, walitambuliwa kuwa ni raia kutoka Eritrea, Algeria, Kongo na Sudan. Likiripoti juu ya kadhia hii, gazeti la Handelsblatt, lilisema idadi hiyo inafanya wahamiaji waliowasili barani Ulaya mwaka huu kufikia watu 68,000 - idadi ambayo ni kubwa kuliko jumla ya wahamiaji 63,000 waliowasili mwaka 2011, kufuatia machafuko yaliyoyakumba mataifa ya Kiarabu.

Likiwa na kichwa cha habari kisemacho: "Kupitia Jahanamu kwenda Mbinguni" Gazeti la Handelsblatt linasema asilimia 90 ya wanaotaka kwenda Ulaya huanzia safari yao hatari nchini Libya, na baada ya kuondoka katika pwani ya nchi hiyo, mengine ni mchezo wa kamari.

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yamezungumzia juu ya wahamiaji haramu wa Kiafrika, miaka mitatu ya uhuru wa Sudan Kusini na matumaini ya amani Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wahamiaji haramu wa Kiafrika waliokolewa baharini.Picha: Filippo Monteforte/AFP/Getty Images

Gazeti hilo lilimnukuu msimamizi wa kituo cha Mare Nostrum kinachosimamia usalama katika bahari ya Mediterrani Admiral Michele Saponaro, ambaye alisema wanaofanya biashara hiyo haramu ya kusafirisha watu wanapochukuwa fedha za wakimbizi hao, hawajali tena iwapo wanawafikisha salama au la.

Serikali ya Italia inaelemewa na mzigo huo wa wakimbizi na waziri mkuu wake Mateo Renzi aliyatolea mwito mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya kusaidia katika kukabiliana na tatizo, ambalo alisema siyo la Italia pekee bali na kanda nzima ya Umoja wa Ulaya, na wanachokifanya wao kinaisadia kanda nzima.

Tabaka la wasoni linaloishi kifahari

Gazeti la die tageszitung liliadika juu ya maadhimisho ya miaka mitatu ya uhuru wa Sudan Kusini na vita vya wenyewe kwa wenye vilivyoiharibu nchi hiyo maskini kabisaa duniani. Gazeti hilo linasema wakati mamilioni ya raia wa Sudna Kusini wakiogelea katika dimbwi la umaskini, wasomi wa tabaka la juu, ambao wengi ni wanasiasa, wanajeshi na wafanyabiashara kutoka chama tawala cha SPLM, wanaishi maisha ya kifahari.

Hivi sasa SPLM na tabaka la wasomi wamegawika tangu mapambano ya madaraka kati ya rais Salva Kiir na hasimu wake Riek Machar yalipogeuka kuwa mgogoro wa kikabila mwezi Desemba. Zaidi ya watu milioni moja wameguezwa wakimbizi na mapigano, na karibu 800,000 wamekimbilia katika nchi jirani. Watu wasiopungua 10,000 wameshauwa katika mgogoro huo.

die tageszeitung linamnukuu Abraham Awolich kutoka kituo cha utafiti cha Sudan Kusini ambaye anasema sababu kuu zilizoko nyuma ya vita hivyo ni rushwa na mapambano ya madaraka, kwa lengo la kudhibiti rasilimali za taifa, na hasa mafuta, ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa hilo.

Rais wa Sudan Kusini wakiadhimisha miaka mitatu ya Uhuru Julai 9.
Rais wa Sudan Kusini wakiadhimisha miaka mitatu ya Uhuru Julai 9.Picha: CHARLES LOMODONG/AFP/Getty Images

die tageszeitung linasema wakati nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 2011, wastani wa kipato cha mtu mmoja mmoja ulikuwa euro 1,350. Kiwango hicho kilikuwa kikubwa kuliko kiwango cha wastani wa euro 550 cha Kenya na mara nyingi zaidi ya kiwango cha euro 350 cha Uganda. Mataifa hayo yote yana maendeleo makubwa kulinganishwa na Sudan Kusini. Lakini kutokana na mapigano, uzalishaji wa mafuta ulipungua na wakati huo huo kiasi kikubwa cha fedha umma zimeibwa na hivyo kipatao cha raia kimepungua maradufu.

Gazeti hilo linasema uongozi wa taifa hilo hivi sasa uko mikononi mwa wasi wa zamani waliopigana vita vya zaidi ya miongo miwili dhidi ya utawala wa Sudan mjini Khartoum. Makamanda wa zamani walibadilisha sare zao kwa suti, na kuanza kuzitumia nafasi zao kujitajirisha bila hata chembe ya aibu, linaadika gazeti la die tageszeitung.

Al-Shabaab yarudi kwa kishindo

Gazeti hilo hilo pia liliandika juu ya kurejea kwa kishindo cha kundi la itikadi kali za dini ya Kiislamu la Al-Shabaab nchini Somalia, kufutia shambulio lililofanywa kwa ustadi mkubwa katikati mw amji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu. Wapiganaji wa kundi hilo walijipenyeza katika eneo la kasri la rais maarufu kama "Villa Somalia" Jumanne jioni, na kuanzisha mapigano yaliyodumu saa kadhaa kati yao na vikosi vya serikali na vile vya Umoja wa Afrika AMISOM.

Alshabaa walisema waliwauwa wanajeshi 14 wa serikali. Gazeti hilo liliandika juu ya mashambulizi yaliyotokea mjini Arusha nchini Tanzania ambamo watu wanane walijeruhiwa, na mashambulizi ya karibu kila siku kwenye maeneo ya pwani ya Kenya, ambayo yanalenga kuilaazimisha nchi hiyo kuondoa wanajeshi wake nchini Somalia.

Wanajeshi wa Somalia wakiangalia mabaki y agari lililoharibiwa na mripuko mbele ya makaazi ya rais mjini Mogadishu.
Wanajeshi wa Somalia wakiangalia mabaki y agari lililoharibiwa na mripuko mbele ya makaazi ya rais mjini Mogadishu.Picha: picture-alliance/dpa

Mshumaa wa matumaini Afrika ya Kati

Mada nyingine iliyopewa kipaumbele katika magazeti ya Ujerumani ni kuhusu matumaini ya kupatikana kwa amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Gazeti la Süddeutsche Zeitung liliropiti kuwa wawakilishi wa makundi ya wanamgambo wa Seleka na anti-balaka watakutana mwishoni mwa mwezi huu mjini Brazaville katika Jamhuri ya Kongo, kujadili makubaliano ya kusitisha uhasama.

Mazungumzo ya awali tayari yanafanyika mjini Bangui kwa muda wa wiki tatu sasa. Waziri wa ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian, aliyaelezea mazungumzo hayo kama mshumaa wa matumaini.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Saum Yusuf