1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan yatia saini mkataba na Marekani

30 Septemba 2014

Afghanistan na Marekani zimetia saini makubaliano leo(30.09.2014) yanayoruhusu majeshi ya Marekani kubakia nchini humo kupindukia mwishoni mwa mwaka huu.

https://p.dw.com/p/1DNpy
Afghanistan Sicherheitsabkommen mit den USA
Sherehe za kutiwa saini mkataba mjini KabulPicha: SHAH MARAI/AFP/Getty Images

makubaliano hayo yanamaliza mwaka mmoja wa hali ya sintofahamu juu ya hali ya baadaye ya majeshi ya kigeni yanayosaidia Waafghanistani wakati wakichukua jukumu la usalama katika nchi yao.

Viongozi wa Afghanistan, Marekani na wa NATO wameyakaribisha makubaliano hayo , ambayo yataruhusu kiasi ya wanajeshi 10,000 wa marekani kubakia nchini humo baada ya ujumbe wa mapambano wa majeshi ya kimataifa kumalizika tarehe 31 Desemba.

Afghanistan Soldat mit US Soldaten 29.03.2014
Wanajeshi wa Marekani nchini AfghanistanPicha: Getty Images/Scott Olso

Rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai alikataa kutia saini licha ya vitisho vya Marekani vya kuondoa kabisa majeshi yake iwapo hakutakuwa na chombo cha kisheria kitakachowalinda wanajeshi wa Marekani.

Maafisa wa Marekani wamesema kuwa uchelewesho huo katika kutiwa saini kwa makubaliano hayo hakutaathiri mipango ya mwaka ujao.

Rais Ashraf ghani Ahmadzai , ambaye aliapishwa kushika madaraka hayo siku moja kabla, ameuambia mkusanyiko huo kuwa makubaliano yaliyotiwa saini yanaashiria hatua muhimu ya mabadiliko kuelekea katika hali bora katika uhusiano wa nchi hiyo na dunia.

"Makubaliano haya ni kwa ajili tu ya usalama na uthabiti wa Afghanistan," amesema.

Afghanistan US Soldaten mit afghanischen Soldaten Archiv 2009 Kabul
Wanajeshi wa jeshi la Marekani na Afghanistan kwa pamojaPicha: picture-alliance/dpa/Marcel Mettelsiefen

"Makubaliano haya ni kwa maslahi ya taifa letu. Makubaliano ya pande mbili ya usalama yatasafisha njia kwa ajili ya Afghanistan kuchukua udhibiti," ameongeza.

Mshauri mpya aliyeteuliwa wa masuala ya usalama nchini Afghanistan , Mohammad Hanif Atmar na balozi wa Marekani James Cunningham walitia saini makubaliano hayo katika ikulu ya rais katika mji mkuu Kabul.

Makubaliano ya pili yanayoruhusu majeshi ya NATO kubakia nchini humo pia yalitiwa saini pia wakati wa sherehe hizo.

Ashraf Ghani Ahmadzai Kabul Afghanistan Porträt
Rais Mpya wa Afghanistan Ashraf Ghani AhmadzaiPicha: picture alliance/AP Photo/Massoud Hossaini

Mtendaji mkuu wa serikali Abdullah Abdullah , ambaye amepewa wadhifa ambao ni sawa na waziri mkuu baada ya kutia saini makubaliano ya kugawana madaraka na Ghani Ahmadzai , pia ameukaribisha mkataba huo wa usalama.

"Umetiwa saini baada ya tafakari ya kina," amesema na kuongeza kuwa " mkataba huo unaojulikana kama BSA si kitisho kwa majirani zetu. Utasaidia kuimarisha amani na uthabiti katika kanda hiyo."

Katibu mkuu wa NATO Anders Fogh rasmussen ameukaribisha mkataba huo , akisema unaainisha ujumbe mpya wa kundi hilo la mataifa kutoa mafunzo, ushauri na kusaidia majeshi ya Afghanistan.

Einigung über Einheitsregierung in Afghanistan unterzeichnet 21.9.2014
Viongozi wawili wenye nguvu nchini Afghanistan , Abdullah Abdullah (kushoto) na rais Ashraf Ghani Ahmadzai(kulia)Picha: AFP/Getty Images

"Tutaendelea kusaidia kutoa fedha kwa majeshi ya usalama ya afghanistan, taasisi zake, na kuendeleza zaidi ushirikiano wetu wa kisiasa na kiutendaji na Afghanistan kupitia ushirikiano wetu wa siku zote," amesema katika taarifa.

Wakati huo huo Waafghanistan katika jimbo muhimu kimkakati upande wa kaskazini wa mji mkuu wametishia kufanya uasi iwapo rais mpya nchini humo hataheshimu makubaliano ya kugawana madaraka na kiongozi waliyemchagua , Abdullah Abdullah.

Gavana wa jimbo la Panjshir Abdul rahman Kabiri amesema watu wanawasi wasi kuwa Abdullah anaweza kutupwa nje ya madaraka.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Josephat Charo